Utata wa Baadhi ya Viambishi Tamati katika Vitenzi vya Kiswahili
Keywords:
Kiswahili, Viambishi, Viambishi Tamati Ishilizi, VitenziAbstract
Baadhi ya viambishi tamati katika vitenzi vya Kiswahili vimechanganuliwa na kuelezwa kwa namna zinazokinzana miongoni mwa wanaisimu mbalimbali. Makala hii inafafanua utata unaojitokeza katika suala hilo na kisha kupendekeza suluhisho muafaka. Makala hii ni matokeo ya utafiti wa mapitio ya machapisho pamoja tajiriba ya elimu ya sayansi ya lugha ya Kiswahili ya mwandishi akiwa na uzoefu wa kufundisha isimu ya lugha ya Kiswahili na Kiingereza chuoni kwa miaka zaidi ya kumi. Aidha, mwandishi anajenga hoja za kimantiki baada ya tafakari tunduizi ya masuala tatanishi huku hoja hizo zikishadadiwa kwa kupanua data husika. Upanuzi wa baadhi ya data ulisaidiwa na wadau wa Kiswahili katika makundi ya WhatsApp ya Kiswahili na isimu. Utata wa ufafanuzi na uchanganuzi unaooneshwa katika makala hii unahusu baadhi ya viambishi tamati ishilizi “a, e, i na u,’’ katika vitenzi vya Kiswahili. Halikadhalika, utata mwingine ni kuhusu viambishi tamati vilivyopata kuchanganuliwa au kubainishwa na wanaisimu waliotangulia. Baadhi ya wanaisimu wamechanganua kwa namna hii: “-eni/-uni/-ini” (mf. lim-eni/thubut-uni/safir-ini) huku wanaisimu wengine wakichanganua hivi: “-ni” (mf. lime-ni/thubutu-ni/safiri-ni). Makala hii imependekeza uchanganuzi na ufafanuzi mpya wa viambishi hivyo: “-en-i” (mf. lim-en-i), “-un-i” (mf. thubut-un-i) na “in-i” (mf. safir-in-i). Katika uchanganuzi huu mpya, viambishi -en-, -un-, na -in- vinarejelea dhana ya upamoja.
Published
How to Cite
Issue
Section

This work is licensed under a Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License.
This work is licensed under a Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License.