Uchanganuzi wa Mofu katika Kauli Mbalimbali za Mnyambuliko wa Vitenzi vya Silabi moja: Lahaja ya Ginantuzu

https://doi.org/10.58721/jkal.v3i2.1151

Authors

Keywords:

Ginantuzu, Kauli za vitenzi, Mfuatano, Mofu, Silabi

Abstract

Suala la mfuatano wa mofu katika kauli za vitenzi limewavuta wanaisimu wengi. Hata hivyo, hakuna utafiti ambao umefanyika katika Kisukuma lahaja ya Ginantuzu kuhusu mfuatano wa mofu katika kauli za vitenzi vya silabi moja. Kwa hiyo, makala hii ililenga kuchunguza uchanganuzi wa mofu katika kauli mbalimbali za mnyambuliko wa vitenzi vya silabi moja katika lahaja ya Ginantuzu. Lengo la makala hii lilikuwa kuchunguza vitenzi vyenye silabi moja na kubainisha mfuatano wa mofu katika kauli za vitenzi katika lahaja ya Ginantuzu. Utafiti ulifanyika katika kata za Sapiwi na Matongo wilaya ya Bariadi Vijijini. Vijiji viwili vilipitiwa na mtafiti. Vijiji hivyo ni Igegu na Matongo. Jumla wa watoataarifa 20 walifikiwa kwa uwiano sawa wa kijinsia. Vitenzi 80 viliteuliwa na mtafiti na kuwekwa katika kategoria mbili; vitenzi visoukomo katika kundi moja na vitenzi vya silabi moja katika kundi jingine na kupelekwa kwa watoataarifa. Watoataarifa waliteuliwa kwa kuzigatia kigezo cha usampulishaji lengwa. Data za makala zilikusanywa kwa mbinu ya Ushuhudiaji, mahojiano, hojaji na mapitio ya nyaraka za maktabani, makavazi na mitandaoni. Kama mwongozo wa kazi hii, makala imetumia nadharia ya Kanuni Tazamishi (KAT). Aidha, Mkabala wa kitaamuli ndio umetumiwa kubainisha mfuatano wa mofu na kauli. Matokeo ya makala ilibaini kauli sita (6) za vitenzi. Jumla ya vitenzi kumi vya silabi moja katika lahaja ya Ginantuzu vilipatikana. Makala pia imeonesha kuwa, baadhi ya vitenzi vya silabi moja havikubali kupokea baadhi ya mofu za kauli husika. Kikanuni, upangaji wa kauli hizi sio wa kubandika tu bali unafuata kanuni ya utokeaji wake.

Published

2025-07-15

How to Cite

Masanja , N. (2025). Uchanganuzi wa Mofu katika Kauli Mbalimbali za Mnyambuliko wa Vitenzi vya Silabi moja: Lahaja ya Ginantuzu. Journal of Kiswahili and Other African Languages, 3(2), 19–29. https://doi.org/10.58721/jkal.v3i2.1151

Issue

Section

Articles