Urefu wa Irabu katika Viambishi-Awali vya Vitenzi Viso-Ukomo vya Kiswahili Sanifu
DOI:
https://doi.org/10.58721/w8d1eq25Keywords:
Irabu, Kiswahili sanifu, Viambishi, VitenziAbstract
Makala hii inawasilisha matokeo ya utafiti iliochunguza iwapo kiambishi-awali cha kitenzi kiso-ukomo, <ku->, kinaweza kuathiri urefu wa irabu pindi kinapoambatishwa kwenye mashina ya utenda ya vitenzi vya Kiswahili sanifu. Utafiti huo wa kitaamuli ulitumia usampulishaji sinasibu na nasibu ili kuteua sampuli zilizotoa data za utafiti. Data zilikusanywa maktabani, katika Chuo Kikuu cha Dodoma, kwa kutumia mbinu ya upitiaji nyaraka; na uwandani, katika eneo la Mji Mkongwe, Zanzibar, kwa kutumia mbinu ya usaili. Data hizo zilikuwa vidahizo vya Kiswahili sanifu vyenye uambishaji kisarufi na uambishaji nyambulishi. Vidahizo hivyo vilitamkwa na wazungumzaji wa Kiswahili sanifu. Matamshi hayo yalirekodiwa kwenye kinasa-sauti na kuchakatwa maabarani kwa kutumia programu ya kompyuta ili kubainisha nyakaa za irabu mbalimbali zinazotokea kwenye matamshi hayo. Uchanganuzi wa data unaonyesha kuwa kiambishi-awali kiso-ukomo, <ku->, kinaweza kuathiri urefu wa irabu za vitenzi kulingana na vipashio vinavyotokea mwanzoni mwa shina la utenda la kitenzi husika, au kulingana na sifa za kitenzi zilizorithiwa kutoka lugha ya Mame-Bantu. Mashina ya vitenzi yanayoanza kwa konsonanti yanapoambatishiwa kiambishi-awali kiso-ukomo, <ku->, irabu zake huendelea kuwa na urefu uleule. Mashina mengi ya vitenzi vinavyoanza kwa irabu <a->, <e->, <i-> na <o-> nayo irabu zake huwa na urefu uleule yanapoambatishiwa kiambishi-awali kiso-ukomo, <ku->. Hata hivyo, kuna vitenzi vichache vinavyoghairi kanuni hiyo, ambapo hukubali irabu ya kiambishi hicho kuyeyushwa na kuwa kiyeyusho cha midomo, halafu irabu inayofuatia ya shina la kitenzi hurefushwa ili kufidia urefu wa irabu iliyoyeyushwa. Kwa mashina yanayoanza kwa irabu <u->, urefu wa irabu za maumbo mapya yanayozaliwa huendelea kuwa uleule yanapoambatishiwa kiambishi-awali hicho. Zaidi ya hayo, kitenzi <kuja> ndicho kitenzi pekee cha Kiswahili sanifu chenye irabu ndefu kwenye kiambishi-awali kiso-ukomo, <ku->. Hata maneno mengine yanayotokana na kitenzi hicho yana irabu ndefu, au konsonanti ndefu, kwenye viambishi-awali vyake, inayopakana na mzizi wa neno, kama ilivyo irabu ndefu katika kitenzi <ku:ja>. Inavyoelekea, Kiswahili sanifu hurefusha irabu au konsonanti inayotokea kabla ya mzizi wa kitenzi <ku:ja>, au kabla ya mzizi wa maneno yanayotokana na kitenzi hicho, ili kufidia silabi ya kwanza ya mzizi wa kitenzi hicho iliyokuwepo katika lugha ya Mame-Bantu.
Downloads
Published
Issue
Section
License
Copyright (c) 2026 Journal of Kiswahili and Other African Languages

This work is licensed under a Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License.
This work is licensed under a Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License.





